Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, akiwa na mkurugenzi wa TPDC, James Mataragio, akiashiria kupokea mchango wa madawati 500 kutoka kwa shirika hilo. |
Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, akiongea na wakazi wa Madimba waliohudhulia hafla ya kukabidhi madawati kwa halmashauri ya wilaya ya Mtwara iliyoandaliwa na TPDC |
Wanafunzi kutoka shule mbalimbali za msingi za kata ya Madimba. |
Mkurugenzi wa TPDC, James Mataragio, akitoa taarifa ya shirika hilo katika hafla ya kukabidhi madawati 500 kwa halmashauri ya wilaya ya Mtwara. |
Na Juma Mohamed, Mtwara.
SHIRIKA la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limekabidhi madawati 500 kwa halmashauri
ya wilaya ya Mtwara kwa ajili ya kusaidia kutatua changamoto ya ukosefu wa
samani hizo katika shule za msingi inayopelekea wanafunzi wengi kukaa chini.
Akizungumza
wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika shule ya msingi Madimba, mkurugenzi wa
shirika hilo, James Mataragio, alisema mchango huo unatokana na shirika hilo
kutambua na kutekeleza kwa vitendo dhana ya uwajibikaji kwa jamii hasa zile
ambazo shughuli za utafiti na uendelezaji wa gesi na mafuta zinafanyika na zile
zinazopitiwa na miundombinu ya gesi.
Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego na mkurugenzi wa TPDC, James Mataragio. |
Alisema,
utekelezaji wa dhana hiyo unalenga kujenga mahusiano bora baina ya jamii na
shirika, yanayojengwa kwenye misingi ya kuboresha huduma na ustawi wa jamii.
“Ni
matumaini yetu kwamba michango tunayoitoa inasaidia kutatua kero mbalimbali za
kimaendeleo katika jamii zetu..katika kuendeleza kutekeleza dhana ya
uwajibikaji, TPDC imechangia madawati 500 kwa halmashauri ya Mtwara vijijini
lengo likiwa ni kumaliza tatizo la wanafunzi kukaa chini wakiwa darasani..”
alisema Mataragio.
Alisema,
mchango huo unatarajiwa kuleta tija baadae kwa wanafunzi kupata elimu bora
pamoja na kupata wataalamu watakaofanya kazi katika sekta ya mafuta na gesi
hapo baadae.
Aidha,
sambamba na mchango huo, shirika hilo pia limekabidhi mfano wa hundi yenye
thamani ya sh. Milioni 150 kwa halmashauri hiyo, ikiwa ni malipo ya tozo za
huduma (Service levy) kwa shughuli za uzalishaji na uchakataji wa gesi.
Mataragio
alisema, malipo hayo ni jumla ya mauzo ya gesi kwa kipindi cha miezi sita toka
mwezi Oktoba mwaka 2015, ambapo watakuwa wakilipa malipo hayo kwa kipindi cha
kila baada ya miezi mitatu ili kuhepuka kukwamisha shughuli za kimaendeleo kwa
halmashauri.
Halima Dendego na James Mataragio (katikati) kushoto ni mbunge wa Mtwara vijijini, Hawa Ghasia na kulia ni mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally. |
“Leo hii
tumeweza kulipa takribani Milioni 150 ikiwa ni tozo ya huduma kwa shughuli za
uzalishaji wa gesi katika halmashauri ya Mtwara vijijini..niwahakikishie kwamba
malipo ya tozo ya huduma yataendelea kukua kadiri uzalishaji wa gesi
unavyokua..” aliongeza.
Akizungumza
katika hafla hiyo, mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, aliushukuru uongozi
wa TPDC kwa mchango huo na kusema kuwa halmashauri ya wilaya ya Mtwara ilikuwa
inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa madawati kama ilivyo kwa halmashauri
nyingine nchini.
“Tulikuwa na
upungufu wa madawati 5,563 kazi ya ukarabati kwa yaliyopo inaendelea na kazi ya
kutengeneza mapya inaendelea, wenzetu wa TPDC leo wamekuja kutuunga mkono kwa
namna ya kipekee kutukabidhi madawati 500 mapya, nani kama TPDC..” alisema.
Wanafunzi wakifurahi katika hafla ya kukabidhi madawati. |
Alisema,
kitendo hicho kimewaongezea mwendo viongozi wa mkoa na wa wilaya katika safari
ya kujinasua katika dhahama ya kutumbuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli ambaye aliagiza mpaka kufikia mwezi Juni
kila mkoa uwe umekamilisha utatuzi wa changamoto hiyo.
Hata hivyo,
alikiri kuwa bado kuna changamoto kubwa katika suala la madawati na kwamba
jitihada zinafanyika kuwasiliana na wadau wengine kuweza kuchangia utatuzi wa
jambo hilo huku akiwataka wawekezaji wengine kuiga mfano wa TPDC katika
kusaidia kutatua changamoto hizo.
Madawati
hayo yatagawiwa katika shule zote za msingi za kata ya Madimba ambapo yatakuwa
yamemaliza tatizo la uhaba wa madawati kwa asilimia 100, huku mengine
yakipelekwa katika shule ya msingi Mkubiru iliyopo kata ya Nalingu ambayo
imepata upendeleo huo kutokana na kufanya vizuri katika kufaulisha wanafunzi wa
darasa la saba na kuongoza mkoa kwa matokeo ya mtihani wa mwaka jana.
No comments:
Post a Comment