Na Juma Mohamed, Masasi.
HOPITALI ya
wilaya ya Masasi, Mkomaindo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo
vinavyotokana na uzazi kwa akina mama kutoka vifo 22 kwa mwaka 2014 mpaka kufikia
vifo 12 ambapo ni sawa na asilimia 45.
Akizungumza
wakati wa ziara ya waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto,
Mhe. Ummy Mwalimu, kaimu mganga mkuu wa halmashauri ya mji Masasi, dkt. Mussa
Rashid, alisema mafanikio hayo yanatokana na umoja uliopo kwa madaktari na wauguzi
wa hospitali hiyo.
Alisema,
sababu nyingine ni jitihada za kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa kujifungulia
katika vituo vya afya na hospitali ikiwa ni pamoja na kuwaeleza athari ambazo
wanaweza kuzipata iwapo watajifungulia majumbani mwao.
“Tumekuwa
tukiwaelemisha watu kwamba uzaliaji wa nyumbani tatizo kubwa na ni hatari,
kwahiyo sasa hivi kumekuwa na mwamko mkubwa sana wa jamii kuzalia katika
hospitali..kitendo hiki cha kuzalia hospitali na kwa akina mama pamoja na
kupewa huduma bure zinazotolewa na serikali kumewezesha sisi kuweza kuwapa
huduma zilizo salama kwao..” alisema.
Dkt. Mussa Rashid |
Aidha,
halmashauri hiyo imeweza kufanikiwa katika utoaji chanjo kwa kiwango kikubwa
kiasi cha kuvuka lengo la Kitaifa la asilimia 95, kwa kuweza kufikia asilimia
96 mwaka jana kutoka asilimia 80 ya mwaka 2014.
“Hiki ni
kiwango kikubwa sana ambacho pia kimevuka lengo la Taifa, lakini kwanini tumeweza
kufanikiwa namna hii, tumeweza kufanikiwa kwasababu tunatumia WAJA hawa ni
Watoa Huduma wa Chanjo wa Jamii katika halmashauri yetu, kwahiyo wanatembea na
kwenda kuwachanja watoto..” alisema.
Mhe. Ummy Mwalimu, akiongea na wagonjwa katika hospitali ya wilaya ya Masasi, Mkomaindo. |
Kwa upande
wake, waziri Mhe. Ummy Mwalimu, alisema serikali ya awamu ya Tano itawapima
waganga wakuu wa mikoa, wilaya pamoja na wale wa vituo vya afya kutokana na
uwezo wao wa kuweza kupunguza vifo vya akina mama wajawazito.
“Ni jambo
ambalo mimi mwenyewe nimejiwekea kipimo Mhe. Rais anipime kwahiyo na hili ndilo
tutawapima waganga wakuu wa mikoa, waganga wakuu wa wilaya na waganga wafawidhi
katika vituo vya afya..” alisema.
No comments:
Post a Comment