Friday, April 1, 2016

DC Mtwara akabidhi madawati 200 shule za sekondari.

Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally.

Na Juma Mohamed, Mtwara.

MKUU wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, amekabidhi madawati 200 katika shule 9 za sekondari katika halmashauri ya mji Nanyamba, ambayo imetumia mapato yake ya ndani kuweza kugharamia samani hizo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi madawati hayo, mkuu wa wilaya aliwataka waku wa shule hizo kuhakikisha madawati hayo yanatunzwa vizuri ili yaweze kudumu kwa muda mrefu na kutumiwa na wanafunzi wengine hapo baadae.
“Nimeambiwa kwamba haya madawati ninayokabidhi yamegharimu sh. Milioni 16.5, kwahiyo wananfunzi haya madawati ninawakabidhi nyinyi, namtunzaji namba moja wa haya madawati ni nyinyi..kwahiyo walimu lazima muwasimamie kwa makini sana wanafunzi wenu ili kuhakikisha haya madawati wanayatumia wao na wadogo zao pia wanakuja kuyatumia..” alisema.
Alimpongeza mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Oscar Ng’itu, kwa kutekeleza agizo lake alilolitoa mwezi Aprili mwaka huu la kumtaka asimamie ukarabati wa madawati yote mabovu ambayo yalikuwa yametelekezwa kwenye vyumba vya madarasa.
Alisema, halmashauri hiyo ilikuwa inakabiliwa na upungufu wa madawati 1387 lakini baada ya kuanza jitihada za kuhamasisha utatuzi wa uhaba wa vifaa hivyo sasa tatizo limepungua mpaka kufikia idadi ya madawati 840.

Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally. 

“Lakini na mimi kama mkuu wa wilaya ninahangaika pekeangu kuhakikisha tunasaidiana kutatua hili tatizo, kuna wadau wengi lakini sipendi kuwataja mpaka watakapoleta yale madawati, wameshaniahidi wataniapatia madawati kwa ajili pia ya Nanyamba na halmashauri nyingine..” alisema.
Alisema, kupitia kampeni yake ya kuhamasisha wadau kuchangia madawati kwa hiyari (Haba na haba hujaza kibaba), amefanikiwa kukusanya kiasi kadhaa cha fedha ambacho hata hivyo hakukitaja, huku akiahidi kutoa madawati 50 ambayo tayari yapo.
Kwa upande wake, afisa elimu sekondari katika halmashauri hiyo, Bumi Kasege, alisema hali ya upatikanaji wa viti na meza kwa shule za sekondari sio nzuri, na kwamba hali hiyo inasababishwa na ongezeko la wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2016 wanaofikia idadi ya 1721 ukilinganisha na waliohitimu kidato cha Nne mwaka jana ambao ni 372.
“Sababu nyingine ni baadhi ya wazazi walikuwa hawatoi michango ya viti na meza miaka ya nyuma kabla ya elimu bila malipo..pia baadhi ya meza na viti vilivyokua vinaletwa na wazazi vilikua sio vya kudumu..” alisema.







No comments: