Madaktari na wauguzi |
Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, akiongea na watumishi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mtwara, Ligula. |
Mhe. Ummy Mwalimu, akiwa katika ziara katika kituo cha afya cha Nanguruwe, halmashauri ya wilaya ya Mtwara. |
Mhe. Ummy Mwalimu, akimtengenezea mgonjwa chandarua katika wodi ya wazazi katika kituo cha afya cha Nanguruwe. |
Mhe. Ummy Mwalimu akiongea na mgonjwa katika wodi ya wazazi katika kituo cha afya cha Nanguruwe, alikokwenda kwa ajili ya ziara ya kikazi kukagua utendaji kazi na kusikiliza kero za wananchi. |
Mhe. Ummy Mwalimu, akimwangalia mtoto mchanga katika wodi ya wazazi, kituo cha afya cha Nanguruwe. |
Mhe. Ummy Mwalimu akiwa na mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, wakisikiliza kero za wananchi katika kituo cha afya cha Nanguruwe. |
Add caption |
Na Juma Mohamed, Mtwara.
HUDUMA za
matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mtwara, Ligula, zilikosekana kwa
muda baada ya madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kugoma kwa kushinikiza
kutatuliwa kwa madai yao ikiwamo kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwatia nguvuni
watu wanaodaiwa kumpiga na kumdhalilisha daktari wa hospitali hiyo, dkt.
Dickson Sahini.
Wakizungumza
mapema leo hospitalini hapo, baadhi ya wagonjwa walisema kuwa toka wamewasili
hakuna huduma yoyote ya matibabu iliyotolewa kwao zaidi ya kupokelewa mapokezi
na kupatiwa cheti kisha kuambiwa wasubiri huku kukiwa hakuna dalili zozote za
kushughulikiwa.
Baadhi ya wagonjwa wakisubiri huduma katika jengo la Kliniki ya macho katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mtwara, Ligula, huku madaktari wakiwa na mgomo. |
“Tumefika ‘reception’
tukaambiwa kwamba subirini kuna kitu kinataka kutokea, tuka kaa kama baada ya
nusu saa hivi ndio baadae wakatukatisha vyeti lakini vyeti tumekata mpaka sasa
hivi hatujamwona daktari wala nini na ule mlango umefungwa kabisa..sasa mimi
nahitaji kwenda nyumbani lakini pale pamefungwa na bima yangu ya afya ipo pale
mimi naondokaje kurudi nyumbani..” alihoji Salma Salumu.
Aliwaomba madaktari
kutoa huduma kwa wagonjwa na kwamba kama kuna matatizo wasiyahusishe na
wagonjwa wengine ambao hawahusiki kwasababu wanaweza kusababisha athari kubwa
kwao kwani wapo ambao wanahitaji huduma za dharula.
Naye, fundi
Salumu ambaye alikuwa anasubiri kutibiwa jicho alisema anapata maumivu
kwasababu aliafanyiwa upasuaji na kushonwa hivyo aliwasili hospitalini hapo kwa
ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi na kuweza kupatiwa matibabu na kuondolewa
uzi ambao alishonwa awali.
Wagonjwa wakisubiri huduma. |
“Sasa hivi
jicho limeshaelemewa kwasababu linakiwa kufanyiwa ‘checking’ nadhani wale
wanapofanya ‘operation’ wanashona, sasa uzi unaniathiri kule kwenye macho, sasa
leo nilitakiwa niutowe huo uzi lakini hapa hakuna huduma na wauguzi wote wako
nje na nimekuja hapa nimeweka cheti change kwenye boksi mle wakaniambia hapa
hakuna huduma wauguzi hawapo..” alisema.
Wakizungumza
mbele ya waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Mhe. Ummy
Mwalimu, baadhi ya madaktari wa hospitali hiyo waliopata nafasi ya kueleza
madai yao walisema kuwa hali ya usalama wao iko mashakani kutokana na
kutokuwapo kwa ulinzi wa kutosha hospitalini hapo huku wengine wakipata vitisho
kutoka kwa wananchi.
Dkt. Hindi
Mastai, alisema usalama wao uko hatarini kwasababu wananchi wanaamini kuwa
madaktari wanafanya kusudi wanapojaribu kuwaeleza mapungufu yaliyopo kwa baadhi
ya huduma kwasababu waliaminishwa na viongozi wa serikali kuwa wanaweza kupata
kila hitaji la matibabu ikiwa kama hospitari ya rufaa.
Alisema,
hali imezidi kuwa mbaya kwao hasa baada ya ziara ya waziri mkuu wa jamhuri ya
muungano wa Tanzania, Mhe. Kasim Majaliwa, ambaye alidai kuwa alipewa taarifa
ambazo sio sahihi na baadhi ya viongozi waliompokea.
Dkt. Hindi Mastai, akiwasilisha hoja. |
“Kwahiyo ile
kauli ya waziri mkuu kwamba ‘you will not change Ligula, Ligula will change you’
napenda niwaambie kwamba waziri mkuu kweli itamchenji kwasababu watu wanalindana,
kwasababu ukiangalia matatizo ya Ligula, upande wa vitendea kazi vya hospitali
inafahamika na taratibu ziko wazi hazifanyiki kwasababu watu wanalindana kule
juu..” alisema na kuongeza;
“Watu
wanalalamikia ubadhirifu wa fedha za hospitali, maana yake mpaka muhasibu wa
mkoa anahusika, upande wa ubadhirifu wa majengo mhndisi anahusika, wafanyakazi
wengi wanalalamikia masilahi yao, vyeo, likizo..” aliongeza.
Akiongea kwa
hisia kali, dkt. Hindi, alisema hospitali hiyo ina watumishi wengine wamekwa
katika vitengo ambavyo hawakustahili kuwapo kutokana na taaluma zao kutokidhi
lakini ni kutokana na kulindwa na baadhi ya wakubwa ambao hata hivyo hakuwataja.
Alisema,
hospitali inakosa kuwa na mabomba ya sindano yenye ukubwa wa cc 10, inakosa
kichomea taka hatarishi na hata mitambo ya kukusanya mapato iliyopo haikidhi
kwasababu pesa zinazokusanywa kwa mwezi hazilingani na hadhi ya hospitali.
“Ile mitambo
ya kukusanya makusanyo ni yakisanii tu, ni watu wanatumia kuiba, hospitali ya
mkoa gani inakusanya 300,000 mhe? Wakati tuna wagonjwa zaidi ya 50 au 70 yani
wakuwahi wanawapa ‘information wrong’ mnakuja mnatufokea sisi..lakini mimi
Hindi hata wakinifukuza kazi nitabaki kuwa dokta na ‘I will go anywhere’ na I’m
not afraid of anybody here’..alisema dkt. Hindi.
Asia Mussa,
alisema kitendo alichofanyiwa dkt. Dickson Sahini ni cha udhalilishaji na
hakuna daktari yeyote aliyefurahishwa nacho na kwamba kwa sasa hawezi kufanya
kazi yake kwa hari kama awali.
Alimuomba
waziri kuangalia namna ya kuwapatia usafiri wa basi ambalo litawasaidia
kuwabeba wanapokwenda na kurudi kazini kama ilivyo kwa baadhi ya taasisi jambo
ambalo litasaidia katika kulinda usalama wao.
Akitoa tamkoa
la serikali juu ya tukio la kupigwa kwa daktari, Mhe. Ummy Mwalimu, alivitaka
vyombo vya dola kutosita kuwachukulia hatua wananchi wote wanaokwenda kinyume
na matakwa ya sheria ili kuwahakikishia watoa huduma za afya usalama na amani
wakati wa kutekeleza wajibu wao.
“Kwahiyo
ninawasihi wananchi wote wanaopatiwa huduma katika vituo vyote vya afya nchini
kuacha maramoja tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kufanya vitendo
vinavyoweza kuwakwaza watumishi wa afya..kwavile inchi yetu inafuata misingi ya
utawala unaozingatia sheria, ni vyema wananchi wakafuata taratibu zilizowekwa
wanapohisi kwamba hawakupatiwa huduma za afya kama wanavyostahili..” alisema.
Waziri aliwaomba
madaktari hao kurejesha huduma kwa wagonjwa hospitalini hapo na kuahidi
kuzifanyia kazi changamoto zao ambazo waliziwasilisha kwake huku akiwaambia
kuwa serikali ya awamu ya tano imejipanga vyema kuhakikisha inapunguza kwa
kiasi kikubwa changamoto hizo ambapo wizara inatarajia kupokea madaktari 10,000
kati ya 30,000 ambao iliomba.
Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, akiongea na watumishi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mtwara, Ligula. |
Madaktari walikubali
kurudi kazini na kuendelea kuwahudumia wananchi ambao walikosa huduma kwa muda
hospitalini hapo.
Aidha,
kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Henry
Mwaibambe, alisema watuhumiwa wawili wanaodaiwa kutekeleza tukio hilo tayari
wamekamatwa na wanatarajiwa kufikishwa mahakani haraka.
Alisema,
walikamatwa usku wa juzi kuamkia jana wakiwa katika harakati za kutaka kutoroka
na kukimbilia nje ya nchi.
“Tumejipanga
vizuri kimkoa na nyie mnafahamu na nadhani mnatuunga mkono, hata hao
tuliowakamata walikuwa wanajiandaa kutoroka kwenda nje ya nchi..tumewakamatia
mahali pabaya sana lakini ni usiku wa saa tisa, kwahiyo hatuwezi kushindwa
naomba tu madaktari mtupe ushirikiano ..” alisema Mwaibambe.
Waziri alitembelea
kituo cha afya cha Nanguruwe, halmashauri ya wilaya ya Mtwara akiongozwa na
mwenyeji wake mkuu wa wilaya hiyo, Fatma Ally, ambako huko alikutana na
changamoto kadhaa zaidi ikiwa ni ukosefu wa maji hospitalini hapo.
Katika kuhakikisha
changamoto hiyo inatatuliwa, mkuu wa wilaya alimtaka mkurugenzi wa halmashauri
hiyo Nachoa Zacharia, aahidi mbele ya waziri ni lini maji yatapatikana
hospitalini hapo ambapo mkurugenzi huyo alisema huduma hiyo itaanza kupatikana
katikati ya mwezi Aprili mwaka huu.
No comments:
Post a Comment