Thursday, March 31, 2016

Hospitali na Vituo vya afya Mtwara vyatakiwa kutumia mfumo wa Ki-Elektroniki.


Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Mhe. Ummy Mwalimu,akiongea na watumishi wa hospitali ya rufaa ya Mtakatifu Benedikto, Ndanda.


Mhe. Ummy Mwalimu akiongea jambo na mkuu wa wilaya ya Masasi, Benard Nduta.


Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, akiwajulia hali wagonjwa waliokwenda kutibiwa katika hospitali ya wilaya ya Masasi, Mkomaindo, wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi na kuongea na watumishi wa hospitali hiyo. 


Ummy Mwalimu, akiwajulia hali wagonjwa.



Na Juma Mohamed, Mtwara.

SERIKALI imeagiza vituo vyote vya afya na hospitali mkoani hapa kuhakikisha zinatumia mfumo wa kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato, ili kuhepusha upotevu wa fedha unaopelekea kuzorotesha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi .
Agizo hilo limetolewa na waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, wakati akizungumza na watumishi wa hospitali ya wilaya ya Masasi, Mkomaindo, ambako alifanya ziara ya kuangalia utendaji, utolewaji wa huduma kwa wananchi na kusikiliza maoni ya watumishi.
Hatua hiyo ilitokana na kufurahishwa na taarifa ya hospitali hiyo iliyowasilishwa kwake na kaimu mganga mkuu wa halmashauri ya mji Masasi, dkt. Mussa Rashid, iliyoeleza kuwa hospitali hiyo imepiga hatua katika ukusanyaji wa mapato kwa siku ambapo awali kabla ya kufunga mfumo wa kielektroniki walikuwa wanakusanya sh. 500,000 huku baada ya kuanza kutumia mfumo huo wanakusanya sh. Milioni 1.5.

Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, akiwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi na kuongea na watumishi katika hospitali ya rufaa ya Mtakatifu Benedikto, Ndanda, wilayani Masasi.


“Kwahiyo Milioni 1 ilikuwa inapotea kwa siku inakwenda wapi, kwa mwezi una Milioni 30 umezipata, kwanini usilipie wazee kama ulivyosema kwahiyo ndio maana tunasema kadiri unavyokusanya ndio maana mnapata fedha za kununua dawa, ndio maana mmeweza kupata fedha za kuwalipia wazee bima ya afya..kwahiyo DOM tunayo kazi twende mpaka ngazi ya vituo vyetu vyote..” alisema.
Aliipongeza hospitali hiyo ambayo ndio pekee kwa mkoa wa Mtwara kutekeleza mfumo huo na kusema kuwa ataitumia kama mfano katika hospitali nyingine ambazo bado hazijaanza kutumia mfumo huo ambao unatumiwa pia na hospitali ya rufaa ya kanda ya Mbeya.
Alisema, hospitali hiyo awali ilikuwa ikikusanya kiasi cha sh. Milioni 50 kwa mwezi lakini baada ya kuanza kutumia mfumo huo sasa inakusanya sh. Milioni 500 mpaka 600.

Ummy Mwalimu, akiongea na kaimu mganga mkuu wa halmashauri ya mji Masasi, dkt. Mussa Rashid.


“Milioni 400 zilikua ‘zinapigwa’ Milioni 500 zinapigwa, kwahiyo sasa nimepata mfano nzuri wa Masasi, kwamba Masasi mlikua mnakusanya 500,000 mara 30 ni Milioni 15 kwahiyo sasa hivi mtakuwa mnakusanya Milioni 45..Milioni 30 zilikua zinaenda wapi, kwahiyo kwakweli huu ni mfano nzuri na niwaahidi kwamba nitautumia ili kuhamasisha hospitali, mikoa na halmashauri nyingine kuiga mfano huu..” alisema.

Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, akiwajulia hali wagonjwa waliokwenda kutibiwa katika hospitali ya wilaya ya Masasi, Mkomaindo, wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi na kuongea na watumishi wa hospitali hiyo. 


Akieleza mafanikio mengine ya hospitali hiyo, dkt. Mussa, alisema ni pamoja na kupungua kwa vifo vinavyotokana na uzazi kutoka vifo 22 vya mwaka 2014 mpaka kufikia vifo 12 mwaka 2015 ambapo ni sawa na asilimia 45 na kupunga kwa kiwango cha maambukizi ya VVU kutoka asilimia 7.2 mwaka 2014 hadi asilimia 5 mwaka 2015.
“Tumeanzisha wodi ya wagonjwa mahututi (ICU) yenye uwezo wa kulaza wagonjwa Wanne kwa wakati mmoja, tumefanikiwa kununua vifaa tiba vya maabara ambavyo ni Biochemistry na Haematological machines ambazomzimeongeza uwezo wa vipimo ambavyo vilikuwa havipimwi kabla, kama vile matatizo ya Ini, Figo na kipimo cha damu (Full Blood Picture)..” alisema.




No comments: