Thursday, February 18, 2016

Vijana Mtwara watakiwa kujiunga katika makundi ya michezo.

Mbunge wa Mtwara mjini, Maftaha Nachuma (Kulia) akifanya mazoezi ya Ngumi (Boxing) na mmoja wa wachezaji wa klabu ya Ngumi ya Mtwara Boxing, alipotembelea kwa ajili ya kukabidhi vifaa vya michezo





Mbunge wa Mtwara mjini, Maftaha Nachuma, akikabidhi msaada wa vifaa vya michezo kwa viongozi wa klabu ya mchezo wa Ngumi (Mtwara Boxing Club), ikiwa ni mwendelezo wa kutekeleza ahadi zake alizowahi kuzitoa wakati wa kampeni


Na Juma Mohamed, Mtwara.

VIJANA mkoani hapa wametakiwa kujiunga na kuanzisha makundi mbalimbali yakimichezo ili waweze kuwarahisishia wadau kuweza kuwaunga mkono kwa kuwapatia misaada mbalimbali kwa ajili ya kuinua vipaji na kuendeleza michezo.
Akizungumza wakati akikabidhi msaada wa vifaa vya mchezo wa Ngumi (Boxing) katika klabu ya Mtwara Boxing Club, mbunge wa Mtwara mjini (CUF) Maftaha Nachuma, alisema vijana wengi wanahangaika kutafuta ajira wakati wakiwa na vipaji ambapo wakiamua kujikita katika michezo itakuwa ni njia sahihi ya kuweza kupata ajira.
Alisema vifaa ambavyo amekabidhi katika klabu hiyo ambayo aliwahi kuwa miongoni mwa wachezaji kipindi cha nyuma, vina thamani ya sh. Milioni 1.2 huku miongoni mwa vifaa hivyo ikiwa ni pamoja na Gloves, Punching pamoja na Head Guard.
“Mimi kama Mbunge nitahakikisha ninawainua vijana wenzangu na pale wanapokuwa na shida hasa za kimichezo ninatumia pesa zangu za mfukoni kuwaletea vifaa ili tuwe na vilabu bora kabisa Mtwara mjini..niwashukuru tu wachezaji wenzangu ambao wamenipa ushirikiano wakutosha na ninasema kwamba sitowaangusha nitaendelea kuwasaidia ili tuendelee kuwa na klabu imara sana.” Alisema.
Maftaha ambaye alijumuika katika mazoezi ya jioni na wachezaji wa klabu hiyo alisema kitendo hicho cha kutoa msaada ni miongoni mwa harakati zake za kutimiza ahadi zake ambazo alizitoa wakati wa kampeni ambapo alidai kuwa michezo inasaidia vijana wengi kuachana na kujihusisha katika vitendo vya uhalifu.
Naye Hamisi Ally, ambaye ni mwalimu wa Boxing katika klabu hiyo, alisema awali kabla ya kupokea vifaa hivyo walikuwa wakicheza bila vifaa na kupelekea wachezaji kuumizana wakiwa mazoezini kwasababu ya kutokuwa na kinga yoyote.
Katika hatua nyingine, mbunge huyo alikabidhi vifaa vingine vya michezo katika klabu ya mpira wa miguu ya Mkanaredi ya mjini hapa ambavyo ni Jezi seti Mbili na Mipira Miwili.
Alisema, changamoto ya uhaba wa vifaa imekuwa ikizikabili timu mbalimbali manispaa ya Mtwara, ambapo ameahidi kukabiliana na changamoto hiyo ambayo anaamini ikifanyiwa kazi itasaidia kuinua michezo.


No comments: