Wajumbe wa mkutano mkuu wa kawaida wa Chama Kikuu cha Ushirika Masasi-Mtwara (MAMCU), wakiwa nje ya ukumbi wa Emirate, wilayani Masasi, baada ya kugomea kuingia ukumbini wakidai kuongezwa posho. |
Na Juma
Mohamed.
WAJUMBE wa
mkutano mkuu wa kawaida wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi-Mtwara (MAMCU), jana
waligomea kuingia ndani ya ukumbi wa mkutano baada ya kutoridhishwa na kiasi
cha posho waliolipwa kwa ajili ya mktano huo wa siku moja.
Wajumbe hao
walikuwa na kauli moja ya kuto ingia ukumbini mpaka uongozi wa chama hicho utakapoakubali
kuongeza posho hiyo ambayo katika mkutano mkuu uliopita uliridhia kuwa iongezwe
kutoka sh. 70,000 mpaka kufikia sh. 100,000 ambayo hata hivyo haikutekelezwa na
baadala yake iliongezwa mpaka kufikia sh. 80,000.
“Mkutano
mkuu walisema kwa siku ni sh. 100,000 na muda wa siku mbili ni 200,000 na sisi
tunavyokuja hapa tunakuwa na mktano wa siku tatu yani semina na mkutano wa siku
mbili kwahiyo tunalipwa kwa siku tatu na tulikubaliana hivyo, lakini leo
tumekuja tumeambiwa haiwezekani na hatukuambiwa ila tumekabidhiwa tu..sasa
kutokana na hayo sisi hatutaki.” Alisema, David Mng’andile, mkaazi wa wilayani
Masasi.
Ukumbi wa mikutano wa Emirate wilayani Masasi, ukiwa hauna watu baada ya awali wajumbe kugoma kuingia ndai kwa ajili ya kuanza mkutano |
Alisema,
waliamua kupokea posho hiyo ya sh. 190,000 ikijumuisha na gharama za usafiri
ambayo ni ya siku mbili kwasababu waliwasili wilayani Masasi ambako ndiko
mkutano huo ulipofanyika, siku moja kabla ya mkutano na kwamba imewasaidia
kulipia gharama za malazi na chakula na kwamba hata wakiambiwa wazirudishe
hawatokubali huku wakiendelea kudai kiasi kilichobaki.
“Tumekuja
hapa na njaa zetu, tumekuja na nauli zetu na tumekula chakula kwa fedha hiyo
kwasababu tumeshinda hapa jana na leo mpaka sasaivi bado hatujanywa chai na
tunangoja hiyo iliyobaki, kama wakisema turudishe haturudishi kwasababu wao
wanapeana posho lakini sisi wanachama wanatupangia wakati sisi ndio wenye
kuamua..” aliongeza.
Naye
Veronica Hussein, kutoka chama cha Umoja ni Nguvu (AMCOS), alisema wana haki ya
kudai fedha hizo kwasababu tayari zilishapitishwa na mkutano mkuu na kuwekwa
kwenye makabrasha ambayo yamegawiwa kwa wajumbe wote wa mkutano huo, na kwamba
bajeti nzima ya mkutano ni sh. Milioni 72.
“Kwakeli
kupata haki zetu ni sawasawa kwasababu ukiangalia gharama walioipanga ni
milioni 72, na hela tuliyopata ni 160,000..lakini mpaka sasaivi hakuna
kinachoeleweka, mimi na wajumbe wenzangu tunachotaka ni haki yetu na sisi lengo
letu ni moja na hatuwezi kubadilika..” alisema.
Baadaye wajumbe
hao walikubali kuingia ukumbini kutokana na ombi lililotoka kwa viongozi wao wa
chama la kutaka hoja zao wazizungumze ndani ya kikao, ili kuokoa muda.
Wajumbe wa mkutano mkuu wa kawaida wa 16 wa Chama Kikuu cha Ushirika Masasi-Mtwara (MAMCU), wakiwa ndani ya ukumbi wa Emirate, baada ya kukubali kuingia kwa ajili ya kuanza mkutano |
Naye,
Mrajisi msaidizi wa chama hicho, John Henjewele, aliwataka wajumbe hao kuwa
watulivu na kuzingatia maamuzi ya kisheria ambayo yaliamriwa kulingana na
uwiano wa mapato na matumizi yanayopatikana kwa mwaka katika chama hicho, kiasi
cha kumfanya Mrajisi mkuu kupunguza posho hiyo na kusaini kiasi cha sh. 80,000.
Baada ya
mvutano huo kati ya wajumbe na viongozi wa chama, hatimaye mkuu wa mkoa wa
Mtwara Halima Dendego, ambaye ndio alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo,
alihitimisha kwa kutoa pendekezo kwamba kuwe na maridhiano ya pamoja kati ya
wajumbe na meza kuu kwamba pendekezo la kulipwa sh. 100,000 lipelekwe kwa
Mrajisi mkuu kwa ajili ya kuidhinishwa.
Alisema kutokana
na kuwa na idadi kubwa ya wajumbe wanaotaka posho iwe kiasi hicho ambao ni
zaidi ya robo tatu ya wajumbe wote, basi kuwe na wigo wa kupendekeza kiasi
hicho ili mrajisi awe na kazi ya kuidhinisha tu na kwamba kutokana na namna
alivyoona mapato yao, hakuna sababu ya kushindwa kulipana kiasi hicho cha
fedha.
“Katika muda
mfupi ambao nimepitia mapato yenu na matumizi, mimi sioni wapi mutashindwa
kulipana hiyo 100,000..lakini kwasababu tunataka twende kwa utaratibu bila
kuvunja sheria, wekeni wigo sasa makamu akapitishe maana mnazo hela za kutosha,
angalau kwa hiyo 100,000 wajumbe wakija wajadili vya kutosha maana na maisha
yenyewe sasa yamepanda..kwahiyo wala hili halihitaji malumbano wala taarifa,
wekeni azimio meza ikapitishe hilo linawezekana..” alisema.
Meza ilikubali
mapendekezo ya mkuu wa mkoa, na kuwataka wajumbe wawe wavumilivu kwa siku moja
ili jumatatu ya Septemba 7 mwaka huu wapatiwe kiasi cha fedha kilichosalia
kukamilisha sh. 100,000 kama walivyopendekeza ambacho ni sh. 40,000 ambazo
watapokea katika jengo la Ushirika mkoa wa Mtwara, jambo ambalo waliliunga mkono.
No comments:
Post a Comment