KOZI YA WAKUFUNZI WA WAAMUZI YA FIFA KUANZA LEO
Kozi
ya wakufunzi wa waamuzi (Futuro III Refereeing Course) ya Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) inaanza leo (Septemba 10 mwaka
huu) jijini Dar es Salaam.
Jumla
ya washiriki katika kozi hiyo itakayoanza saa 3 asubuhi kwenye hoteli
ya Holiday Inn ambao wanatoka katika nchi 21 za Afrika ni 69. Kozi hiyo
inayotarajiwa kumalizika Septemba 22 mwaka huu inafanyika katika maeneo
mawili ya ufundi (technical) na utimamu wa mwili (fitness).
Nchi
washiriki ni Afrika Kusini, Botswana, Eritrea, Ethiopia, Gambia, Ghana,
Kenya, Lesotho, Liberia, Malawi, Mauritius, Namibia, Nigeria,
Seychelles, Sierra Leone, Somalia, Swaziland, Tanzania, Uganda, Zambia
na Zimbabwe.
Washiriki kutoka Tanzania kwenye kozi hiyo ni Joan Minja, Leslie Liunda na Soud Abdi (technical) na Riziki Majalla (fitness).
Baadhi
ya wakufunzi wa kozi hiyo wanaotoka FIFA na Shirikisho la Mpira wa
Miguu Afrika (CAF) ni Carlos Henriques anatoka Afrika Kusini, Fernando
Gracia (Hispania), Steve Bennett (Uingereza), Tarek Bouchamaoui
(Tunisia), James Sekajugo (Uganda), Bester Kalombo (Malawi), Felix
Tangawarima (Zimbabwe) na An-Yan Lim Kee Chong (Mauritius).
Kozi
hiyo itafunguliwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), Leodegar Tenga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya
Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), mjumbe wa Kamati ya
Utendaji ya CAF na mjumbe wa Kamati ya Vyama (Associations Committee) ya
FIFA.
SERENGETI BOYS YAENDELEA KUJINOA MBEYA
Timu
ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys)
inaendelea vizuri na kambi ya mazoezi mkoani Mbeya ambapo tayari
imecheza mechi moja ya kujipima nguvu.
Ilicheza
mechi hiyo jana (Septemba 8 mwaka huu) dhidi ya Tanzania Prisons
iliyoko Ligi Kuu ya Vodacom kwenye mji wa Nakonde ulioko mpakani mwa
Tanzania na Zambia. Timu hizo zilitoka sare ya 1-1 huku bao la Serengeti
Boys likifungwa na Miraji Selemani.
Serengeti
Boys leo jioni (Septemba 9 mwaka huu) inatarajia kucheza mechi nyingine
wilayani Mbozi dhidi ya Mbozi United. Itacheza mechi ya tatu Jumanne
(Septemba 11 mwaka huu) jijini Mbeya dhidi ya timu ya daraja la kwanza
ya Mbeya City.
Kwa
mujibu wa Kocha wa timu hiyo, Jakob Michelsen kambi hiyo inaendelea
vizuri, na anatarajia kupata mechi moja ya kirafiki ya kimataifa kabla
ya kucheza mechi ya mashindano na Misri, Oktoba 13 mwaka huu Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment